Kwa mujibu wa taarifa ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Rais wa Kolombia, Gustavo Petro, katika ushiriki wake wa nne na wa mwisho kama rais wa Kolombia kwenye Mkutano Mkuu, alisisitiza kuwa Marekani “ni mshirika wa mauaji ya halaiki, kwa sababu haya ni mauaji ya halaiki na jambo hili lazima likemewe mara nyingi na mara nyingi zaidi.”
Aidha, alisisitiza juu ya kuanzishwa kwa vikosi maalumu vya kulinda amani na alipendekeza kuwa vikosi hivyo visiwe chini ya Baraza la Usalama, bali vianzishwe kupitia kura ya maoni katika Mkutano Mkuu, na badala ya majeshi ya kofia za buluu, viwe ni “jeshi lenye nguvu kutoka nchi ambazo hazikubali mauaji ya halaiki.”
Rais wa Kolombia alikumbusha kuwa diplomasia “katika suala la Ghaza imefikia kikomo” na akakosoa kutochukua hatua kwa jumuiya ya kimataifa, Petro anajulikana kuwa mmoja wa wakosoaji wakali zaidi wa mienendo ya utawala wa Kizayuni na miongoni mwa mambo aliyofanya ni kuunga mkono kesi ya Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki na kusitisha mauzo ya makaa ya mawe ya Kolombia kwenda Israel.
Katika hotuba yake pia alipinga mashambulizi ya Marekani katika maji ya Karibiani karibu na Venezuela na akaeleza kuwa siasa ya Washington ya kupambana na madawa ya kulevya ni “chombo cha kutawala mataifa ya Kusini.” Aidha, alisisitiza tena juu ya ulazima wa kukomesha utegemezi wa mafuta na kushughulikia kwa haraka mgogoro wa hali ya hewa.
Hotuba ya Petro ilitolewa baada ya misimamo ya viongozi wengine akiwemo Luiz Inácio Lula da Silva na Gabriel Boric, ambao wote walikosoa vikali kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Ghaza na kusisitiza juu ya ulazima wa kukomesha mauaji ya Wapalestina wasio na hatia na kuelekea katika suluhisho la mataifa mawili.
Maoni yako